 |
| Nyonge nyongeni haki yake mpeni |
|
|

Mauaji ya watu yanayofanywa na mamlaka za
serikali pasipo kufuata sheria pamoja na vurugu zinazohusiana na makundi
na uchawi vimegharimu maisha ya mamia ya Watanzania katika kipindi cha
kwanza cha 2013, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam.
Wakati baadhi ya viashirio vinaonyesha kuboreka kwa kiasi
ikilinganishwa na miezi sita ya kwanza mwaka uliopita, matokeo ya jumla
ya kituo hicho yameibua wasiwasi kwamba Watanzania wanajichukulia sheria
mikononi na kupuuza sheria iliyopo.
Vurugu za vikundi zilisababisha mauaji ya watu 597 katika kipindi cha
nusu ya kwanza ya mwaka huu, ikiwa ni ongezeko kutoka vifo 563 kati ya
Januari na Juni 2012, LHRC ilisema katika taarifa yake ya nusu mwaka
iliyotolewa tarehe 29 Julai. Watu wengi kadri ya 303 waliuawa katika
vurugu zilizohusiana na uchawi katika kipindi cha miezi sita ya kwanza
ya 2013, ikipungua kutoka 336 katika kipindi kama hicho cha mwaka
uliopita.
Katika vurugu za kuua ambazo zilitokea kipindi cha miezi sita ya
mwanzo ya mwaka huu, polisi wa Tanzania, wanamgambo na vikosi vya jeshi
waliwaua raia 22, ambapo raia waliwaua polisi wanane wakiwa kazini, LHRC
iliripoti.
"Mwaka uliopita, watu 31 waliuawa katika mauaji yaliyofanywa na
vyombo vya serikali pasipo kuzingatia sheria mwaka mzima" Mwansheria na
mtafiti wa LHRC Pasience Mlowe aliiambia Sabahi. "Miezi sita ya mwaka
huu, tayari watu 22 wameshauawa. Kiwango kinaidaiwa kuongezeka."
Ripoti hiyo ilionyesha ongezeko la mauaji kutokana na fikra za haki
za makundi, ulinzi hafifu wa haki za raia,ukiukaji wa uhuru wa
kukusanyika, na kukosa taarifa, ni miongoni mwa mambo mengi.
Mlowe alisema kwamba LHRC ilikusanya idadi kwa ajili ya ripoti yake
kutoka polisi, wanaharakati wa haki za binadamu na vyanzo vingine rasmi.
Hivi vinajumuisha ripoti za makamishina wa wilaya ambazo LHRC ilitumia
kubainisha majina ya waathirika na kupata ukweli wa msingi kuhusu
mauaji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Watanzania wanapambana na polisi wakati
wanapohisi kwamba haki zao zinakiukwa, jambo linalosababisha hali hiyo
kuongezeka kwa haraka na kusababisha mauaji.
Kama mfano, ripoti ilinukuu mauaji ya tarehe 11 Januari ya maofisa
wawili wa polisi kwa kupambana na ghasia za madereva wa pikipiki,
zinazojulikana kama boda boda, katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Maofisa hao waliuawa katika ulipizaji kisasi kwa polisi kurusha mabomu
ya machozi katika msongamano wa waandamanaji tarehe 9 Februari.
Kwa kuongezea, ripoti inasema, wahalifu wa siku zote hawawatambui
maofisa wa polisi kama mawakala wa utekelezaji wa sheria na wanajibu kwa
vurugu kubwa wanapokabiliwa. Kwa hiyo, kutumia udhibiti zaidi, maofisa
wa polisi wanatumia nguvu za ziada wakati wa kukabiliana na umma, kwa
mujibu wa ripoti.
Pia imetaja mapigano kati ya madereva wa boda boda na polisi katika
mkoa wa Mtwara mwishoni mwa Januari ambayo yalisababisha vifo vya raia.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini, vurugu zilianza wakati
madereva walipopinga kukamatwa kwa dereva mwenzao wa boda boda na
kuingia mitaani kupinga.
"Hatua ya waendesha boda boda ilikuwa kufanya fujo, zikisababisha
uharibifu mkubwa ambapo majengo ya umma,mali za CCM [Chama Cha
Mapinduzi] na zile za viongozi wao zilichomwa moto," ripoti hiyo
ilisema. "Katika kuchukua hatua, polisi walitumia nguvu kupita kupambana
na wafanya fujo na kusababisha vifo vya watu tisa na 11 kujeruhiwa
vibaya."
Suala la uchawi linazidi kuongezeka
Ripoti iligundua kwamba idadi ya vifo kuhusiana na uchawi inaendelea kuongezeka nchini Tanzania, hususani mkoani Shinyanga.
Pamoja na vifo 303 vinavyohusiana na uchawi katika nusu ya kwanza ya
mwaka huu, tatizo linaongezeka kufikia viwango vya mwaka 2012, wakati
watu 630 walipouawa. Waathirika waliuawa kutokana na tuhuma kutoka kwa
wanajamii wenzao kwamba wamewaroga watu.
Sheria ya Uchawi Tanzania, ambayo inakataza kitendo hicho, inaueleza
uchawi kama "ushirikina, urozi, kufanya uchawi, matumizi ya vifaa vya
kichawi, tendo la kukusudia la nguvu zozote za kiini macho na kukusudia
kumiliki maarifa yoyote ya kiini macho."
Ripoti inadhania kuwepo kwa uchawi katika mgongano wa maslahi ya
kiuchumi kati ya familia zilizo jirani, hususani katika kanda ya ziwa.
"Watu wanarogana wenyewe kwa wenyewe ili kudhibitiutajiri wa familia
[au ukoo]," ripoti ilisema. "[Pia] kiwango kikubwa cha wasiosoma na
imani za kishirikina na kuwatumia waganga wa kienyeji [inachangia katika
mauaji]."
Ripoti inasema ukosefu wa huduma za msingi za matibabu kunachochea mamlaka na imani ya watu kwa waganga wa kienyeji.
Mwanasheria na mjumbe wa timu ya utendaji ya LHRC Imelda Lulu Urrio
alisema ukimya wa serikali katika masuala hayo ulikuwa unasaidia
kuchochea imani za kishirikina na kuwahamasisha wakosaji kufanya mauaji
haramu.
"Kama haitazuiliwa mapema, inaweza kuishia kusababisha mauaji ya watu wengi na kusababisha mauaji ya kimbari," aliiambia Sabahi.
Mwanasheria Harold Sungusiya, ambaye anaongoza programu ya utetezi na
mabadiliko ya LHRC, alisema serikali inapaswa kushughulikia uchawi na
mauaji yanayohusiana na uchawi, vinginevyo itasababisha machafuko
nchini.
"Mtu yeyote anayechukua sheria mkononi kwa kuwaua watu walioshutumiwa
anavunja sheria," Sungusiya aliiambia Sabahi. "Ndiyo, wananchi wanaweza
kuwa na imani ya msingi kwamba uchawi unafanyika lakini wanapaswa kuwa
na imani katika mfumo wa sheria."
Sheikh Ali Mohamed Hemed, imam wa Msikiti wa Kisiwani huko Dar es
Salaam, alisema viongozi wa dini wanapaswa kuwajibika kwa kiasi kikubwa
katika kuuelimisha umma.
"Quran na Biblia zinawakataza kuwaua binadamu wenzenu," aliiambia
Sabahi. "Tunapaswa kufanya zaidi kama watumishi wa dini kuwaongoa
wafuasi zaidi kama njia ya kuistarabisha jamii yetu."
Mchungaji Kamala Simon wa Kanisa la Kilutheri huko Dar es Salaam alisema chanzo cha tatizo kilikuwa kuharibika kwa maadili.
"Tumepoteza mwelekeo wa imani, hivyo watu hawathamini maisha tena,"
alisema Simon. "Kama viongozi wa dini tunapaswa kufanya [jitihada] zaidi
kuirejesha nchi tulikotoka. Tunastahili amani bila ya vurugu."
Watanzania lazima wazingatie sheria
Kikundi cha utetezi wa haki za binadamu kilipendekeza kwamba wananchi
wafuate sheria na kuheshimu mamlaka yaliyotolewa kwa polisi kama
wasimamizi wa sheria. Iliagizwa kwa mashirika ya kusimamia sheria
kuheshimu haki za binadamu na kutumia nguvu zinazotakiwa pale
zinapohitajika. LHRC pia waliomba serikali iingilie kati haraka kesi
zinazohusu uchawi.
Mbunge Ismail Aden Rage aliiambia Sabahi mzizi wa vurugu ulikuwa ni
ukosefu wa uelewa wa jinsi kila mwananchi anavyotimiza wajibu katika
kulinda haki za binadamu na uhuru wa wananchi.
Kwa mfano wakati wa maandamano, ni wananchi gani wanaweza kufanya kwa
haki, sheria za kushiriki zinapaswa kufuatwa ili kuhakikisha usalama wa
vyama vyote, alisema.
"Watu wetu sasa wanaandamana dhidi ya hospitali, Benki Kuu na wakati
mwingine ikulu," alisema Rage. "Viongozi wetu wa kisiasa wana wajibu wa
kuwaelimisha wanachama wao [kutoyakabili] mashirika yetu ya kusimamia
sheria."
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi alisema
serikali imepokea ripoti ya LHRC na kwamba baada ya upitiaji wa kina
itatoa mpango wa utekelezaji kuhakikisha kwamba sheria na haki za
wananchi zimezingatiwa na kulindwa.
"Kitu cha msingi ni utawala wa sheria," Nchimbi aliiambia Sabahi.
"Watu wote wanapaswa kufuata sheria ya nchi, na hakutakuwa na mauaji
kama hayo. Kama serikali tutahakikisha kwamba hili linatekelezwa."