![]() |
| Burundi na Uganda |
Iwapo anatarajia maswahiba wake (Burundi na Uganda)
kumsaidia,
basi ajue vile vile Tanzania
nayo inao marafiki wema ambao
nao hawatasita kujitokeza kusaidia.
Tanzania na Rwanda, zimekuwa na uhusiano mzuri kwa
muda mrefu, lakini uhusiano huu umeanza kuingia dosari pale Tanzania
ilipoamua kuingilia mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
pale ilipokitaka kikundi cha M23 kiondoke katika nchi hiyo ya Afrika ya
Kati.
Majirani wote wa DRC wanajua kinachoendelea katika
nchi hiyo lakini kila mmoja ameamua kukaa kimya. Ni Rais Jakaya Kikwete
aliyeamua kuvunja ukimya na kutoa kauli iliyozua chuki baina yake na
Rais Kagame wa Rwanda.
Chuki zaidi za Kagame dhidi ya Kikwete zimeibuka
pale Tanzania ilipoamua kupeleka majeshi yake ndani ya DRC kwa
mapendekezo ya UN kwa ajili ya kulinda amani katika kifungu cha saba,
kinachoruhusu kujibu mashambulizi pale askari wa kulinda amani
wanaposhambuliwa.
Hiki ndicho chanzo cha Rais Paul Kagame wa Rwanda kuanza kutoa matamshi ya kejeli bila kujielewa dhidi ya Tanzania na rais wake.
Kuna madai kwamba M23 imekuwa ikichukua madini
nchini DRC na kuyapeleka Rwanda kwa makubaliano maalumu na Serikali ya
Kagame. Kama madai hayo ni kweli, basi ni wazi kuwa M23 inasaidia kwa
kiasi kikubwa uchumi wa Rwanda kukua kwa haraka.
Hata hivyo, lawama hizo zote za bure, maana si
Tanzania pekee iliyopeleka majeshi kulinda amani DRC, kwani majeshi ya
Afrika ya Kusini, Msumbiji na Malawi nayo yapo nchini humo.
Bila shaka Rais Kagame anaona sasa ile njia ya
kukuza uchumi wa Rwanda kupitia DRC itakuwa ngumu, hivyo akaona njia
pekee ni kupambana na Rais Kikwete bila kujali kuwa mtazamo wake ulikuwa
ni kuwasaidia wananchi wa Congo, ambao wanateseka muda mrefu kwa na
majeshi ya M23.
Ikumbukwe kuwa kilichomuondoa aliyekuwa Rais wa
nchi hiyo, Mobutu Seseseko, ni kikundi cha Banyamulenge kilichofadhiliwa
na nchi za Uganda na Uganda pamoja na Marehemu Laurent Kabila, baba
yake Rais wa sasa wa Congo, Joseph Kabila, na wanajeshi wa nchi hizo
waliokuwa Tanzania muda mrefu.
Marehemu Kabila alikaa kwa muda mfupi sana
madarakani na yakajitokeza matatizo kati yake na washirika wake
Banyamulenge (Rwanda/Uganda), na mara zikaanza vurugu na hatimaye vita
rasmi na kupeleka mashambulizi Goma kuelekea Kinshasa hadi Kabila
alipoomba msaada kutoka Zimbabwe na Angola.
Majeshi ya nchi hizo za Angola na Zimbabwe
yalifanikiwa kuyarudisha nyuma majeshi ya Rwanda na Uganda ingawa
baadaye waasi walifanikiwa kujipenyeza na kumuua Rais Kabila, ingawa
walishindwa kumweka kibaraka wao kama walivyo kusudia, na nafasi yake
kuchukuliwa na mwanaye Joseph Kabila ambaye naye amekuwa na misimamo
isiyoyumbishwa hadi leo.
Historia ya Tanzania tangu enzi za rais wa Kwanza
wa Tanzania Mwalimu JuliusNyerere, ilikuwa kulisaidia Bara la Afrika na
watu wake kupata amani, na ndicho alichoonekana kufanya Rais Kikwete
DRC.
Chokochoko za Kagame wa Rwanda zinafanana na zile za Idd Amin
Dadaa wa Uganda mwaka 1978 alipotoa maneno ya kejeli kwa nchi yetu na
hatimaye kutuma majeshi yake kuvamia sehemu ya nchi hii kwa madai kuwa
ni mali ya Uganda.
Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa msimamizi wa amani
ya Afrika, alichoshwa na aliyoiita dharau kipindi kile na akatangaza
vita dhidi ya Uganda.
Nyerere alipoamua kupigana na Idd Amin alimwambia
“War is not a dance” (vita siyo muziki) na ndivyo ilivyokuwa kwani
majeshi ya Tanzania yalifanikiwa kuyarudisha nyuma majeshi ya Uganda
chini ya rais wao mvamizi, Idd Amin Dadaa.
Namshauri Rais Kagame, kabla ya kuamua kuingia
vitani na nchi yetu afanye uchunguzi wa kutosha ili baadaye asije
akayajutia maamuzi yake.
Aelewe kuwa Tanzania ni nchi kubwa sana na pia ina
idadi kubwa ya wananchi wenye mapenzi na nchi yao ambao hawatakaa kimya
na kusubiri aitukane na kuonyesha dharau kwao.
Iwapo anatarajia maswahiba wake (Burundi na
Uganda) kumsaidia, basi ajue vile vile Tanzania nayo inao marafiki wema
tu ambao nao hawatasita kujitokeza kusaidia.
Kagame akae akijua kuwa, kujenga nchi ni kazi kubwa inayofanywa kwa miaka mingi, lakini kuibomoa ni dakika moja tu.
Asithubutu kuichezea nchi yetu kwani hakuna Mtanzania atakayekaa kimya akimsubiri aivuruge amani yetu.
(Mwandishi wa makala haya ni mwanajeshi mstaafu.)

No comments:
Post a Comment