Wednesday, 14 August 2013

SPIKA MAKINDA AWATAKA WABUNGE KUTOPOKEA RUSHWA

 
 
 
 
 
 
 
 
SPIKA MAKINDA AWATAKA WABUNGE
 KUTOPOKEA RUSHWA




SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Anne Makinda (MB), amewataka wajumbe wa kamati za Bunge kuachana na tabia ya kupokea bahasha (rushwa) kwa kuwa itachangia kuiuza nchi.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya wajumbe wa kamati tatu za Bunge za Serikali za Mitaa (LAAC), Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Bajeti, Makinda alisema kuwa ni vyema wajumbe wa kamati hizo wakatumia nafasi waliyokabidhiwa kwa ajili ya kutoa huduma za msingi kwa wananchi.

Alisema kuwa iwapo wabunge watashindwa kuwa waadilifu na badala yake wakaendelea kupokea bahasha hizo kuna hatari ya kuiuza nchi na hivyo kutaka tabia hiyo ikome mara moja.

“Iwapo sisi wabunge katika kamati zetu hatuwi waadilifu, ndugu zangu tutakuwa tunaiuza nchi hii, naomba bahasha, tafadhali, zikome mara moja kwa upande wetu,” alisema.

Akitolea mfano, Makinda alisema kuwa Bunge la Uingereza liliwachukulia hatua kwa kuwafungulia kesi za jinai wabunge wake waliobainika kupokea mapato ya udanganyifu/ ziada.

Spika Makinda alisema kuwa ni vyema wabunge wakatunza maadili yao kwa kuwa masuala kama hayo yanaweza kutokea, kwamba wakionyesha mfano mzuri hata wanaotoa bahasha wataogopa na kuweka hesabu zao vizuri.

No comments:

Post a Comment