Thursday, 8 August 2013

DR. MWAKYEMBE : AWASHUKIA WANAOWASAIDIA WAUZA UNGA

DR. MWAKYEMBE : AWASHUKIA
 WANAOWASAIDIA WAUZA UNGA 


Madawa ya kukevya

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewataka watendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), kuachia ngazi endapo dawa za kulevya zitavushwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) bila wao kujua.

Waziri huyo aliyasema hayo wakati akizindua kamati ya nne ya kitaifa ya usalama wa usafiri wa anga, katika ukumbi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) jijini Dar es Salaam.
Mwakyembe ambaye aligoma kusoma hotuba yake aliyoandaliwa kwa ajili ya uzinduzi huo, alisisitiza kuwa endapo tukio kama hilo litatokea tena ni bora watendaji hao wakajiweka tayari kujiondoa mapema kabla hajawafikia.

Dk. Mwakyembe amesema ni aibu na jambo la kushangaza kuona dawa zinavushwa wakati watendaji hao wapo, hivyo akawataka kujiwajibisha kwanza kabla ya hatua nyingine kufuata dhidi yao.
Alisema suala la ulinzi na usalama katika viwanja vyetu ni fedheha na kashfa kubwa iliyoikumba nchi kutokana na kupitishwa kirahisi kwa dawa za kulevya kwenye JNIA, ambao unabeba jina la Baba yetu wa Taifa.

“Tusitafute visingizio katika hili, huu ni udhaifu mkubwa ambao umetuletea ‘udhaifu’ mkubwa kitaifa,” alisema.
 

No comments:

Post a Comment