Pasipo ‘Haki Ardhi’ amani itatoweka
![]() |
| Baragumu |
Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (Udasa), juzi iliandaa kongamano ambalo mada yake kuu
ilikuwa Mustakabali wa Amani na Usalama wa Wananchi Tanzania Miaka 50
Ijayo. Kongamano hilo lilikuwa la kusisimua kutokana na washiriki wengi
kuchangia mada hiyo kwa hisia kali, huku wakielekeza lawama nyingi kwa
Serikali kwamba inatumia Jeshi la Polisi kupora haki za raia, ikiwa ni
pamoja na kukandamiza vyama vya upinzani.
Wachangiaji wengi walisema amani katika nchi yetu
katika miaka 50 ijayo iko shakani kutokana na kutokuwapo kwa demokrasia
ya kweli, hali ambayo walisema inaweza kusababisha vita huko tuendako.
Jambo la kushangaza ni kwamba wachangiaji karibu wote waliona masuala
yenye sura ya kisiasa kama ndio yatakuwa chanzo cha uvunjifu wa amani
hapa nchini katika miaka 50 ijayo.
Suala la ardhi halikuzungumzwa, ingawa ndilo suala
kubwa zaidi ya mengine linaloweza kuingiza nchi yetu katika machafuko
iwapo masuala ya umiliki ardhi, kero na migogoro inayohusu ardhi
haitapata suluhisho. Suala la ardhi limekuwa likipuuzwa na Serikali na
Bunge pasipo kujua kwamba ardhi ndiyo itakayoamua hatima ya nchi yetu.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba ardhi ni rasilimali ya msingi katika
uzalishaji. Hivyo, haki ya kumiliki ardhi ni njia ya kuhakikisha kuwapo
kwa usalama na amani katika jamii.
Pamoja na suala la umiliki wa ardhi kuingizwa
katika Katiba, bado kuna changamoto nyingi katika sekta ya ardhi ambazo
zimeleta malalamiko mengi. Hizi ni pamoja na migogoro ya ardhi, kuchukua
ardhi ya wananchi bila ridhaa yao na kulipa fidia ndogo isiyoendana na
thamani ya ardhi.
Limejitokeza tatizo la wanasiasa kuwapora wananchi
ardhi. Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia ya kaya zenye hatimiliki ya
ardhi ni ndogo na inaendelea kushuka, wakati kesi zinazohusiana na
migogoro ya ardhi zinaongezeka. Kulingana na Sensa ya Utafiti wa Kilimo
(ACS) ya mwaka 2007/2008, idadi ya kaya za vijijini zinazomiliki ardhi
kwa kutumia hati rasmi imeshuka kutoka asilimia 7.1 mwaka 2002/2003 hadi
asilimia 5.8 mwaka 2007/2008.
Takwimu za Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi
zinaonyesha kuwa, idadi ya migogoro ya ardhi ambayo kesi zake
zimefunguliwa imeongezeka kutoka 1,490 mwaka 2004/5 hadi 40,088 mwaka
2011, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2,590. Hii sio ishara njema kwa
mustakabali wa nchi yetu, kwani kuporwa kwa ardhi kunakofanywa na
wanasiasa na vigogo serikalini ni jambo la hatari kwa amani yetu.
Hivyo, lazima Serikali isiyafumbie macho madhara
ya kuchukuliwa kwa maeneo makubwa yaliyosababisha kushuka kwa umiliki wa
ardhi miongoni mwa kaya za vijijini na kuongezeka kwa kesi za migogoro
ya ardhi. Pia suala la kulipa fidia stahiki na kwa haraka kwa ardhi
iliyonyakuliwa ni suala linalohitaji kufanyiwa kazi hivi sasa.
Inashangaza kuona kuwa, pamoja na Katiba na sheria za nchi kutaka fidia
ya haki na haraka, mamlaka husika zimekosa utashi na hivyo matakwa hayo
hayatekelezwi.
Utashi wa kisiasa ndani ya Serikali na Bunge
unahitajika katika kutekeleza matakwa ya ‘Haki Ardhi’. Vinginevyo, nchi
yetu itaingia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe huko tuendako, kwani
historia imeonyesha kwamba hakuna mwananchi anayekubali kufa njaa kwa
kukosa ardhi, huku wengine wakiwa wamejilimbikizia ardhi kubwa
wasiyoihitaji.

No comments:
Post a Comment