Spika asiwagwaye
wabunge walarushwa
Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe
kuliongoza Bunge la Kumi baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 amekiri kwamba kuna tatizo kubwa la rushwa miongoni mwa wabunge na amezitaka Kamati za Kudumu za mhimili huyo wa dola kufanya kazi kwa uadilifu pia kuwataka wabunge kuacha vitendo vya kudai na kupokea rushwa.
Spika Makinda alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa wiki
mjini Bagamoyo, mkoani Pwani alipokuwa akifungua mafunzo ya wajumbe wa
Kamati za Hesabu za Serikali Kuu (PAC), Serikali za Mitaa (LAAC) na
Bajeti ambayo yaliandaliwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG). Tofauti na wakati wowote katika kipindi cha
uongozi wake wa chombo hicho cha kutunga sheria, mara hii Spika Makinda
alipata ujasiri na kusema wabunge wakome kuomba na kupokea rushwa, huku
akionya kwamba iwapo watashindwa kuwa waadilifu wataiuza nchi.
Kwa tafsiri yoyote ile, kauli ya Spika Makinda ni
nzito na ni bahati mbaya kwamba aliitoa katika mkusanyiko wa wabunge
wachache badala ya kikao cha Bunge zima.
Tunasema hivyo kwa sababu inaweza ikatafsiriwa kwa
makosa kwamba Spika alikuwa akiwalenga tu wabunge wa Kamati hizo tatu
za Bunge wakati ukweli ni kwamba alikuwa akielekeza fadhaa zake kwa
wabunge wote wa Bunge la Kumi ambalo yeye ndio kiongozi.
Pengine jambo ambalo hakulitilia maanani ni kwamba
ujumbe wake ungekuwa na uzito zaidi iwapo angeutoa katika kikao mwafaka
cha kuzungumzia rushwa katika Bunge ambacho kingehudhuriwa na wabunge
wote. Bila shaka kikao hicho kingewapa wabunge wote fursa ya kujikosoa
na hatimaye kuondoka na msimamo wa pamoja dhidi ya wabunge walarushwa.
Wapo watu wanaosema kwamba kauli ya Spika Makinda
imetolewa ikiwa imechelewa na kuhoji alikuwa wapi muda wote huo hadi
akaitoa wakati Bunge la Kumi likikaribia kumaliza muda wake. Hoja yao
kuu ni kwamba samaki mkunje angali mbichi na wanamlinganisha Spika na
mtu anayetafuta shuka kujifunika kukiwa kumekucha. Wakosoaji wanawaona
wabunge walarushwa katika Bunge hili kama watu walioharibika kiasi cha
kutorekebika kwa kuwa Bunge hilo liko katika kipindi cha lala salama.
Hoja za wakosoaji wa Spika kwa kweli ni za msingi.
Wanasema katika uongozi wake, Spika Makinda alipata fursa tele za
kutokomeza vitendo vya rushwa, lakini alishindwa kuzitumia. Alizima
sauti za wabunge waliokuwa wakilalamikia vitendo vya rushwa vya baadhi
ya wabunge. Ndio maana ni vigumu kumsahau Mbunge wa Kigoma Kusini, David
Kafulila alipolieleza Bunge Juni 13, 2011 namna wabunge wa Kamati ya
LAAC walivyokuwa wakipokea rushwa kutoka kwa watumishi wa Serikali, huku
akiwataja kwa majina baadhi ya wabunge aliodai aliwakamata ‘live’
wakiwa wanafanya hivyo.
Pamoja na kumkabidhi Spika ushahidi wa tukio hilo,
hadi sasa kiongozi huyo hajachukua hatua yoyote. Baada ya muda mfupi
mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo ambaye pia alitajwa na Kafulila
alikamatwa akidaiwa kupokea rushwa katika tukio tofauti na kufunguliwa
kesi ambayo bado iko mahakamani.
Madai hayo ni mbali na madai ya rushwa dhidi ya
wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo Spika aliivunja
lakini pia akashindwa kuchukua hatua.



No comments:
Post a Comment